Mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, leo amekumbana na adhabu ya Bunge kutokana na kitendo alichokifanya cha kuonesha kidole cha ‘kati’ ndani ya Bunge, ishara inayotafsiriwa kuwa tusi.

Mwenyekiti wa kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika ameliambia Bunge kuwa Kamati yake ilipokea malalamiko kuhusu kitendo cha mbunge huyo kuonesha ishara ya matusi bungeni, Juni 3 mwaka huu katika kikao cha 37, mkutano wa tatu wa Bunge la 11.

Alisema kuwa shtaka hilo lilitokana na muongozo ulioombwa na Mbunge Jacquline Msongozi ambaye alieleza kuwa alimshuhudia kwa macho yake mbunge huyo wa Mbeya mjini akinyoosha kidole cha kati ambacho kinaashiria tusi, wakati akitoka bungeni, muda mfupi baada ya kuanza kwa mjadala wa Wizara ya Habari, Utamaduni,  Michezo na Sanaa kuhusu dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Mkuchika alisema kuwa Kamati yake ilimhoji Mbunge huyo ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo ambaye alikiri kunyoosha kidole hicho cha kati.

Alisema katika utetezi wake, Mbunge huyo alidai kuwa wakati anatoka nje ya Bunge alimsikia mbunge mmoja wa CCM akimtukana matusi ya nguoni na ya mama yake hivyo alipata hasira na kujikuta akinyoosha kidole hicho.

Hata hivyo, ingawa tafsiri iliyotolewa kuhusu ishara hiyo ni tusi linalomaanisha kuingilia kinyume cha maumbile, Sugu alieleza kuwa haina maana ya moja kwa moja kama ilivyotafsiriwa na kwamba hutumika pia kama ishara ya kupinga jambo.

“Nakumbuka nilionyesha mkono wa vidole viwili ambayo ni body direction, kidole cha kati ni resistance sign inawezekana nilinyoosha kidole cha kati kwa sababu ya temper,” Mkuchika alimnukuu Sugu.

Mkuchika alisema kuwa baada ya kupitia hukumu zilizowahi kutolewa na nchi mbalimbali kwa kosa hilo, Kamati yake iliamua mbunge huyo asihudhurie vikao 10 vya Bunge.

Nyundo ya kamati hiyo pia imempiga mbunge wa Ubunge, Saed Kubenea ambaye amedhibiwa kutohudhuria vikao vitano vya Bunge kuanzia leo. Kubenea alikutwa na hatia ya kutoa maneno ya uongo dhidi ya Waziri Hussein Mwinyi na kutomuomba radhi.

Wabunge hao wanaungana na wabunge wengine wa upinzani ambao wanaendelea kutumikia adhabu ya kukosa vikao vya Bunge ikiwa ni pamoja na Zitto Kabwe na John Heche.

''Tanzia'' Mwandishi Maarufu Nigeria Afariki
Mr. Blue: Bifu kama ni la Chuki halina Maana