Bondia Seleman Kidunda, aliitwa muoga, wapo waliodiriki kumuita kunguru, majina mzaha kwake ya hayakuishia hapo kutokana na wapo ambao waridiki kumuita bondia anayepewa mabondia wengi wa kawaida, kwa lugha ya mtaani, wanasema ndizi.
Kidunda amepokea lawama hizo baada ya kushindwa kupanda ulingoni katika pambano ambalo lilipangwa kupigwa Februari 24, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar, kutokana na kuelezwa kuugua siku chache kabla ya pambano halo.
Bondia huyo ambaye ni muajiriwa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) akiwa na cheo cha sajini taji ‘staff sergent’, alikuwa katika wakati mgumu kabla ya kujitokeza hadharani kuwaomba msamaha wadau wa ngumi huku akieleza ukweli wa afya yake kutetereka.
Kutokana na kukosekana kwa Kidunda katika pambano hilo, wengi walitegemea itamchukua muda mrefu kupata pambano kutokana na kuwaangusha watu wengi kwa kushindwa kupanda ulingoni, lakini Kampuni mpya ya promosheni ya ngumi za kulipwa nchini, PAF Promotion Company Limited ikaamua kumpa kazi maalum Juni 30, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es salaam.
Kidunda anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Eric Mukadi kutoka DR Congo katika pambano ambalo limepewa jina la ‘Hata Usipolala Patakucha’.
Siku hiyo pia Mfaume Mfaume ‘Mapafu ya Mbwa’ atapanda ulingoni kwenye pambano la utangulizi dhidi ya Nkululeko Mhlongo wa Afrika Kusini.
Kidunda amezungumzia pambano hilo ambalo linatarajia kuwa na upinzani mkali kutokana na muhusika kupewa majina mengi ya kejeli licha ya kwamba ana rekodi ya kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola katika ngumi za ridhaa.
Kidunda anasema: “Nataka nikwambie kwamba namshukuru Mungu, naendelea na maandalizi ya pambano kwa kufanya mazoezi makali kwa sababu najua halitokuwa pambano jepesi kutokana mpinzani mwenyewe.
Mukadi amesema anakuja kukufundisha ngumi?
“Hayo ni maneno yake hayawezi kunitisha na nisingependa kuongelea anachokisema zaidi ya mimi kujikita kwenye maandalizi kwa sababu atakavyokuja ndivyo tukakavyompokea.
Unadhani ni rahisi kumpiga Mukadi?
“Kwa nini isiwe rahisi? Nadhani unaujua ubora wangu na ninavyokuwa kwenye ringi (ulingo), sasa kwa nini asipigike kama nafanya mazoezi kwa ajili yake.
“Muda mrefu sana sijapanda ulingoni tangu baada ya pambano langu na Katompa, nilipata pambano ila sikufanikiwa kupigana kutokana kupata changamoto ya kuumwa, ukweli ilinisikitisha sana ila sasa huyu ndiye anaenda kupokea ile adhabu niliyoshindwa kuitoa.
Inaonekana Mukadi anakufahamu vizuri kutokana na uhakika wake kwamba atakupiga?
“Sijui katika hilo, lakini ninachotaka kukwambia kwa sasa mashabiki wangu waje kwa wingi Mlimani City hiyo Juni 30, nataka waje waangalie burudani ya ngumi na siyo maneno kama anavyosema mpinzani wangu.
Unarudi Mlimani City kwa mara ya pili ukienda kucheza pambano kuu, nini unaweza kuwaambia mashabiki wako?
“Kitu kikubwa waje kuijaza Mlimani City, waje wakiwa wamenunua mabaga ya kutosha na kuku kwa ajili ya kuangalia burudani kubwa ambayo nitaitoa, huku wakiwa wanakula baga zao na kuku walionunua kwenye migahawa ya pale Mlimani City.
Vipi KO itapatikana kweli? “Kawaida yangu huwa silazimishi KO, inakuja yenyewe kutokana na kupiga mbavu na kidevu, sasa ikitokea itakuwa vizuri kwa sababu ni pambano moja pekee ndiyo sijashinda kwa KO.