Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Seleman Kidunda ameweka wazi kuwa sasa yupo tayari kupanda ulingoni dhidi ya, Patric Mukala aliyeambiwa amekimbia kwani kwake anaona hana maajabu yoyote ya kumshangaza.
Kidunda ametoa kauli hiyo baada ya kumbamiza Eric Mukadi wa DR Congo katika pambano lililopigwa kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es salaam, Ijumaa (Juni 30).
Ikumbukwe mwezi Februari, mwaka huu Kidunda alishindwa kupanda ulingoni dhidi ya Mukala kutokana na madai ya kuwa mgonjwa, lakini ilitafsiriwa kama amemkimbia bondia huyo kutoka Afrika Kusini mwenye uraia wa DR Congo.
Kidunda amesema kitendo cha yeye kumtaka bondia yeyote, alikuwa anamanisha anataka aletewe, Mukala ambaye aliambiwa amemkimbia kitu ambacho hakikuwa na ukweli wowote.
“Nilivyosema nataka waniletee bondia yeyote nilimaanisha kwamba kwa sasa nipo tayari niletewe yule Mukala ambaye walisema nimemkimbia, jambo ambalo halikuwa na ukweli wowote.
“Unajua yule hana maajabu yoyote kwangu isipokuwa bahati mbaya alinikuta nikiwa mgonjwa na hakuna mtu ambaye alitarajia kuwa nitaumwa, ila kwa sasa wamlete nimuonyeshe kazi halafu watu waelewe kwa nini Kidunda ndiyo nusu mtu, nusu Jini,” amesema Kidunda.