Baada ya kuziacha alama tatu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Mabingwa watetezi Young Africans, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amewaangushia lawama wachezaji.

Mtibwa Sugar ilikubali kupoteza mchezo huo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufungwa 3-0, huku ukiwa mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu huu.

Kifaru amesema Wachezaji wao hawakuonesha uwezo wa kupambana dhidi ya Young Africans, hali iliyopelekea kutoa nafasi kwa wenyeji kumiliki mpira muda mwingi na kujikuta wakipoteza kwa idadi kubwa ya mabao.

Amesema matarajio ya Uongozi wa Mtibwa Sugar yalikua makubwa kabla ya mchezo huo kutokana na uwezo waliouonesha katika michezo mitatu iliyopita, lakini ilikua tofauti katika mchezo wa jana Jumanne (Septemba 13).

“Tulikua na matarajio makubwa ya kuona tukiendelea kucheza soka la ushindani ambalo tulilionesha katika michezo mitatu iliyopita, imekua tofauti sana kwa sababu wachezaji wetu walicheza chini ya kiwango na kutoa nafasi kwa Young Africans kumiliki mpira kwa muda mrefu.”

“Kwa upande mwingine ninaweza kusema wachezaji wetu walikua na wasiwasi na hili halikuwa jambo zuri kwao kwa sababu walijiandaa kukabiliana na Young Africans, naamini kocha Mayanga ameliona hili na atalifanyia kazi hili ili turudi katika kiwango chetu, ila ninaendelea kusema hatukupaswa kupata matokeo haya.” amesema Kifaru

Mabao ya Young Africans katika mchezo huo yalipachikwa nyavuni na Beki wa kulia Djuma Shaban, Mshambuliaji Fiston Mayele pamoja na Kiungo Mshambuliaji Aziz Ki.

Kenya: Polisi yatuhumiwa kushambulia raia uapisho wa Ruto
Waziri Mkuu arushiwa lawama mlipuko Chuo Kikuu