Uongozi wa Mtibwa Sugar umesema hautegemei viingilio vya milangoni kama ilivyo kwa baadhi ya klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza.
Mtibwa Sugar wametoa kauli hiyo kupitia idara yao ya Habari na Mawasilino inayoongozwa na Thobias Kifaru ambapo wamesisitiza kuwa mpango huo wataendelea nao, licha ya Wadau wengi wa soka kuwashangaa baada ya kuanza kuutumia Uwanja wa Manungu Complex.
Mchezo uliopita Mtibwa Sugar iliwakaribisha Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na ulimalizika kwa sare ya bila kufungana, huku wadau wengi wa Soka wakishangazwa na Uwanja huo kukosa sifa ya kuwa na majukwaa.
Kifaru amesema:”Hatutegemei mapato ya mlangoni ili kuweza kuendesha timu yetu kwa kuwa tuna bajeti ya miaka 40 kwa ajili ya kuweza kuendesha timu yetu hii.”
“Sisi Uwanja wa Manungu ni mzuri na bora tumeufanyia maboresho na umepitishwa kwamba unafaa kutumika kwenye mechi za ligi.”
“Kikubwa ni kuweza kuwapa mashabiki burudani na mechi zetu zitachezwa hapa bila mashaka yoyote yale tupo tayari na tutazidi kupambana,” amesema Kifaru.