Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na makundi yanayosimamia uhuru wa vyombo vya Habari wamejipanga kuandaa hafla ya kumbukumbu ya mwanahabari aliyeuwawa mwaka jana, Jamal Khashoggi.
Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika mjini Instabul leo, nje ya ubalozi wa Saudi Arabia ambapo inaaminika kuwa ndipo alipo uawa mwanahabari huyo.
Maadhimisho hayo ya mwaka mmoja baada ya kifo chake yamepangwa pia kufanyika muda sawia na ule alioingia katika ubalozi wa nchi yake ili kupata nyaraka za kumuoa mpenzi wake wa kutoka Uturuki, Hatice Cengiz.
Siku ya tukio, Cengizi (37), alikaa nje ya ubalozi kwa saa kadhaa akimsubiri mpenzi wake kabla hajagundua kuwa ametoweka.
Kwamujibu wa taarifa kutoka nchini Uturuki zinaeleza kuwa khashoggi aliuawa na kukatwakatwa na kikosi cha mauaji cha Saudi Arabia baada ya kuingia katika ubalozi huo.
Hadi sasa hakuna mtu aliyeshtakiwa kuhusiana na kifo cha Khashoggi licha ya kuwa Uturuki na idara za ujasusi kutoka mataifa ya Magharibi zinaeleza kuwa agizo la kumuuwa linaonekana kutoka katika uongozi wa juu wa Serikali ya Saudi arabia.