Madaktari na Wauguzi wanane waliokuwa wakihusika na uangalizi wa nguli wa soka Diego Maradona watafikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa makosa ya uzembe katika kifo cha mwanasoka huyo maarufu Duniani.
Jaji mmoja ameamuru kusikilizwa kwa kesi ya mauaji bila kukusudia baada ya jopo la madaktari kubaini matibabu ya Maradona yalijaa ‘mapungufu na dosari’.
Maradona alifariki mnamo Novemba 2020 kwa mshtuko wa moyo huko Buenos Aires, akiwa na miaka 60 licha ya kuwa alikuwa akipata nafuu nyumbani kutokana na upasuaji wa kuganda kwa damu kwenye ubongo mapema mwezi huo.
Siku chache baada ya kifo chake waendesha mashtaka wa Argentina walianzisha uchunguzi kuhusu madaktari na wauguzi waliohusika katika uangalizi wake.
Mwaka jana, jopo la wataalam 20 walioteuliwa kuchunguza kifo chake liligundua timu ya matibabu ya Maradona ilifanya “njia isiyofaa, yenye upungufu na ya kutojali”.