Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africansumeweka wazi mpango wa kufanya usajili kabambe ili kuhakikisha msimu ujao klabu hiyo inaendelea kufanya vizuri katika Michuano ya ndani na nje ya Tanzania.
Young Africans imejizatiti kufanya hivyo, baada ya kuibuka kinara wa mafanikio kwa misimu miwili mfululizo, ikitwaa Ngao ya Jamii, Ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, huku msimu uliopita ikitinga Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kupoteza mbele ya USM Alger ya Algeria.
Mmoja wa Viongozi wa Young Africans amesema mipango hiyo imeanza baada ya kufanikisha kumpata Kocha Mkuu Mpya, Miguel Angel Gamondi ambaye anakuja kurithi mikoba ya Nasreddine Nabi aliyeondoka mwishoni mwa msimu wa 2022/23.
Amesema jambo kubwa kwa sasa klabuni hapo ni kuhakikisha wanawabakiza mastaa wao ambao bado wana umuhimu mkubwa kwa timu akiwemo Mshambuliaji hatari Fiston Kalala Mayele.
“Young Africans kama viongozi tumefanya kazi nzuri msimu uliopita na tunafurahi kuona timu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, hivyo ambacho tunakifanya kwa sasa ni kuhakikisa msimu ujao tunayafikia mafanikio ambayo tuliyafikia msimu uliopita.
“Kikubwa tunachotaka kukifanya ni kuhakikisha tunafanya usajili wa maana ambao utaongeza nguvu kwenye kikosi chetu, lakini pia kuwabakisha wale wote ambao ni muhimu kwa timu, watu wanatakiwa kuwa watulivu na watashuhudia vyuma vya maana vikitua Young Africans katika dirisha hili linalokuja la usajili,” amesema kiongozi huyo
Hadi sasa Young Africans imeshatangaza kuachana na Wachezaji watano ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi chao kwa msimu ujao 2023/24.
Wachezaji hao ni Bernard Morrison, Dickson Ambundo, Tuisila Kisinda, Abdallah Shaib ‘Ninja’ pamoja na Mlinda Lango Erick Johora.