Serikali ya Tanzania imepokea mkopo wa masharti nafuu wa Dinar milioni 4.5 sawa na shilingi bilioni 33.9 kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (KFED), kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa umwagiliaji katika bonde la mto Luiche mkoani Kigoma.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya fedha na Mipango, Benny Mwaipaja.

Mwaipaja alisema kuwa Mkataba huo umesainiwa nchini Kuwait kati ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Aisha Amour, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa KFED, Abdulwahad Ahmed Al- Bader, kwa niaba ya Serikali ya Kuwait.

“Fedha hizo za mkopo zitatumika katika uhakiki wa usanifu wa kina wa mradi na usimamizi wa ujenzi wa bwawa la maji la mita 375 lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo milioni 70 za maji”, alisema Mwaipaja.

Amesema kuwa fedha hizo pia zitatumika katika ujenzi wa miundombinu kama mifereji ya maji, kinga za mafuriko, daraja na barabara zitakazotumika kutoa huduma zenye urefu wa kilometa 21.

Mradi huo unategemewa kuongeza wigo wa kilimo cha umwagiliaji katika eneo la takribani hekta 3,000, na kutoa fursa za ajira mbalimbali kabla na baada ya kuanza kutekelezwa

TCRA Yatoa adhabu ya bilioni 11.8
Wasifu wa kocha mkuu Young Africans - Zlatko Krmpotic