Waziri wa maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, amesema ameridhishwa na kasi ya ukarabati wa barabara za mamlaka ya hifadhi Ngorongoro (NCAA) zilizokuwa zimeathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Na amewahakikishia wadau wa utalii nchini kuwa eneo hilo liko salama kwa wageni kufanya utalii bila shida yoyote.

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya NCAA, na kutembelea kreta ya Ngorongoro iliyokuwa na changamoto ya barabara kutokana na kujaa maji.

Dkt. Kigwangalla amesema ” Tulipata athari ya kuharibika barabara kadhaa ndani ya kreta kutokana na mvua zilizonyesha kwa miezi mitano mfululizo, hapo mwanzo katibu mkuu wa wizara yetu, Profesa Adolf Mkenda alikuja kushauriana na wataalamu na juhudi kubwa zilianza kuboresha barabara”

Ameongeza kuwa ” Tungeweza hata kuweka lami barabara za eneo lote la kreta kwakuwa hatuna changamoto ya kibajeti, lakini lazima eneo hili libaki na uhalisia (nature) wake wa mazingira ya asili ambayo huwezi kuyapata sehemu nyingine duniani.

Kamishna wa uhifadhi mamlaka ya hifadhi Ngorongoro, Dkt. Freddy Manongi amesema kazi kubwa ya ukarabati wa miundombinu imefanyika ili kutoathiri shughuli za utalii isipokuwa kipande kidogo chenye urefu wa kilomita 1.5 ndio kilichofungwa kwa muda ili kujaza kifusi na kuweka makalavati ya kutoa maji.

NIDA washusha mitambo kufyatua vitambulisho 9,000 kwa saa
Mwanafunzi darasa la saba afungishwa ndoa kwa Ng'ombe 10