Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii  ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Vijijini Hamis Kigwangalla amemshukru Rais Dkt. John Magufuli kwa kumuamini kama msaidizi katika Wizara za Afya na ya Maliasili na Utalii katika awamu iliyopita ya uongozi wake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Kigwangala ameandika:-

“Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai, miaka mitano iliyopita haikuwa rahisi kwangu, ilikuwa miaka ya kupanda na kushuka ya kusimama na kuanguka ya kujaribu na kufanya, kukosea na kupatia

Ni kipindi kilichojaa furaha na maumivu, uhai na umauti, ni kipindi nilichonusa kifo na kufufuka, ni kipindi nilichoshangilia na nilicholia machozi, ni kipindi nilichopata ulemavu wa milele na maumivu yasiyoisha wala kusahaulika

Siwezi kumlalamikia Mungu kwa lolote lile zaidi namshukuru kwa kuwa hai na kwa nyakati zote nilizopitia za kiza totoro na za mwangaza, kipindi hiki nilipewa heshima ya kuwa msaidizi wa Rais kwa nafasi nyeti Serikalini (Afya na Maliasili na Utalii)

Naomba nitumie fursa hii kumshukuru Rais, Dr. John Pombe Magufuli, kwa imani yake kubwa kwangu, kwa maelekezo na usimamizi wake, si tu alikuwa Kiongozi wangu mkuu bali pia alikuwa Mwalimu na Baba, sintosahau huruma na upendo alionionesha nilipopata ajali na msiba wa mwanangu

Rais alipokea machela yangu huku akilia machozi, alihakikisha usalama na matibabu yangu wakati wote, ninawashukuru pia Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa uongozi na usimamizi wao wa karibu, kipekee ninawashukuru sana watumishi wote wa sekta za Afya na Maliasili niliohudumu nao kipindi nikiwa serikalini

Tumepata mafanikio makubwa sana kwa uwezo wao na kwa kujitoa kwao, mara zote walinipa ushirikiano wa dhati kama moja ya viongozi wakuu wa sekta hizo, ninawashukuru sana wadau wote wa sekta nilizohudumu

Mara zote nilipokutana nao niliwasikiliza kwa umakini na kushughulikia changamoto walizokuwa nazo, kimsingi walikuwa dira ya kazi zangu, hata hivyo, mimi ni binadamu dhaifu, sijakamilika, naomba radhi kwa kila niliyemkwaza ama kumuumiza

Haijawahi kuwa lengo langu bali ni jitihada za kujaribu kufanya mambo yafanikiwe, kazi ya kufanya jambo liwe zuri na timilifu siyo rahisi, Mimi sina kinyongo na mtu na naomba sana niliowakwaza wanisamehe” ameandika Kigwangala.

Aidha, Kigwangala amempongeza Dkt. Damas Ndumbaro kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na kueleza kuwa anatarajia kumkabidhi Ofisi kesho Desemba 10, 2020.

“Nimempongeza Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Maliasili na Utalii na nakusudia kesho kwenda kumkabidhi rasmi ofisi, nawapongeza Mawaziri wote na nawaahidi ushirikiano wangu wakati wote” ameandika Kigwangalla.

Tangu Rais Magufuli alipoteua Baraza Jipya la Mawaziri Desemba 5, ambapo Mawaziri kadhaa waliokuwepo katika Baraza la Mawaziri lililopita akiwemo Kigwangala hawajarejeshwa katika Baraza jipya la Mawaziri, kumekuwa na mashambulizi ya maneno katika mitandao ya Kijamii yakielekezwa moja kwa moja kwa Kigwangala.

Wakati wa Uongozi wake katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Kigwangala alionekana kujibu hoja mbalimbali zilizohusu majukumu yake kupitia mitandao ya kijamii na wakati kampeni za uchaguzi mkuu zilipopamba moto, Sakata la Klabu ya Simba kumteua Barbara Gonzales kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Simba SC nalo lilipamba moto huku Kigwangala akionekana kulipa kipaumbele zaidi suala la Simba akihoji uteuzi wa Barbara na Sakata la ‘Bilioni 20 za Mo Dewji’.

Kufuatia sakata hilo Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bashiru Ally alimuonya Kigwangala akimtaka kujihusisha zaidi na kampeni za chama chao kuliko masuala ya Simba SC.

Lakini si Kigwangala pekee ambaye hajarejeshwa katika Baraza jipya la Mawaziri, wapo wengine ambao ni pamoja na Isaac Kamwelwe aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Angela Kairuki aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Japhet Hasunga aliyekuwa Waziri wa Kilimo  na Luhaga  Mpina aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Ghana: Mahama atahadharisha kuhusu wizi wa kura
Magufuli asamehe wafungwa 3316, "Bora ninyongwe mimi"