Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangalla ameitetea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukanusha kwamba haijaizuia vibali vya kuingiza ndege mpya kampuni ya Fastjet Tanzania inayomilikiwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri Kigwangalla amesema kwamba kwa taarifa alizonazo ni kuwa kampuni ya Fastjet imeshindwa kufanya biashara nchini na sio inavyosemekana kuwa imezuiwa kuingiza ndege mpya na serikali.
Masha akizungumza na chombo cha habari kimoja amesema TCAA inasema ili aweze kuingiza ndege ni lazima amalize kwanza madeni yake yote.
Hata hivyo Mamlaka ya Usafiri Tanzania (TCAA) imesema inaidai Fastjet zaidi ya Shilingi Bilioni 6.
”Tayari tumemaliza lakini fedha imeisha kwa kuwa tayari fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa yao wangeniruhusu nifanye kazi ili nipate fedha kulipa madeni yaliyobaki” Amesema Masha.
”Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba wameshindwa kufanya biashara wao wenyewe na hakuna sababu ya kuwazuia kuingiza ndege yao mpya ni kwamba wazungu wamejiondoa wamebaki wazawa hawajazuiliwa kuingiza ndege zao” amesema Kigwangalla.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya anga, Hamza Johari amesema Notice hiyo inaanza Disemba 17 hadi Januari huku akitoa tahadhari kwa wananchi kutotumia usafiri wa shirika hilo ili kuepuka usumbufu.
Hata hivyo Mamlaka imezuia ndege hiyo ya Fastjet isiondoke hapa nchini kutokana na madeni makubwa yanayodaiwa na shirika hilo.