Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema ameamua kumfuta katika orodha ya marafiki zake, mfanyabiashara maarufu nchini na mwekezaji wa Klabu ya Simba, Mohammed Dewhi baada ya kutofautiana.
Kigwangalla amesema hayo wakati akihojiwa na Edwin Odemba wa Star TV ambapo amedai kuwa aligundua uwezo wa kufikiri wa mfanyabiashara huyo ni mdogo baada ya kuanika kuwa alikwenda kumkopa pikipiki, alivyonyimwa mkopo huo ndipo Kigangallah akaanza kumponda Mo Dewji mitandaoni akimtaka aondoke Simba.
“Sijamtafuta Mo Dewji kwa sababu nilimfuta miongoni mwa marafiki. Mimi mtu akizingua ninaondoka. Ukileta kutonuheshimiana wakati mimi nakuheshimu, hapo hapo ninaachana na wewe.
“Mo Dewji alinidharau, na ningeenda mbele ningemchukulia hatua za kisheria, kwa sababu alinichafua kisiasa lakini nilimpuuza. Niligundua uelewa mdogo sana, uwezo wake ni mdogo wa kufikiria.
“Huwezi kwenda ukasema huyu alinikopa, kwenye biashara hatufanyi hivyo. Wangapi wangetamani kwenda kuomba mkopo kwake? Yeye mwenyewe anakopa, mimi nina taarifa zake za mikopo lakini siwezi kuweka hadharani, ni private.
“Mimi na yeye ni mashabiki wa mpira, lakini kuna ndugu zake dada yake, mama yake, baba yake, hawana ugomvi na mimi. “Nikisema niishtaki ile biashara ili nilipe fidia nitakuwa nimewaumiza na wengine ambao hawahusiki.
“Yeye alipaswa kutenganisha biashara yake na ushabiki wake na Simba. Anafanya biashara inayohusiha familia nzima, sio yeye peke yake. Kwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikiria asingesema maneno kama yale, kwa hiyo nilivyoona kaongea vile nikampuuza,” amesema Kigwangalla