Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka viongozi wa Jumuia ya Tawala za Mitaa (ALAT) kuhakikisha wanatekeleza haraka mfumo wa anuani za makazi
Kijaji ameyasema hayo alipokua akifungua semina ya kuwajengea uelewa wajumbe wa ALAT na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo wa Anuani za Makazi jijini Dodoma Septemba 29,2021.
Dkt Kijaji amewathibitishia wajumbe kuwa zaidi ya sh. bilioni 40 zimetengwa katika wizara hiyo kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Anuani za Makazi lakini pia katika wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuna fedha zimetengwa kwa ajili hiyo.
Amewaomba wajumbe wa ALAT kila eneo walipo waunganishe nguvu kusaidia kuutekeleza haraka mfumo huo wa Anuani za Makazi ili ifikapo mwaka 2025 uwe umekamilika katika ngazi zote nchini.