Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia Imani Mbilinyi (25) mkazi wa kijiji cha Maleutsi, Wilaya ya Makete Mkoani Njombe kwa tuhuma za mauaji akituhumiwa kumpasua kichwa babu yake aitwaye Elia Mbilinyi (90) na kisha kuutoa ubongo wake karibu na nyumbani kwao.
Tukio hilo la kikatili limetokea usiku wa kuamkia Oktoba 14, 2020 majira ya saa mbili usiku ambapo inatajwa kuwa mtuhumiwa baada ya kutekeleza mauaji hayo aliamua kujisalimisha kwa Mwenyekiti wa mtaa wa Luswaganga katika kijiji hicho.
“Jana tulipewa taarifa kwamba kijana huyo amefanya maujai ikabidi tumkamate na kutoa ripoti kituo cha polisi na walichukua jitihada za kututafuta na kumchukua mtuhumiwa,kwakweli tuligundua mzee amelala amechokonolewa ubongo na uzuri wake kijana alipofanya mauaji alikuja kujieleza yeye mwenyewe kirabuni” amesema Michael Mnzengwasanga, Afisa Mtendaji kijiji cha Maleutsi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Usadanga, Exavery Mbilinyi yalikotokea mauaji hayo, amesema baada ya kuelezwa taarifa hizo aliamua kuwaita mgambo wa kijiji wakamuweka chini ya ulinzi na kisha wakatoa taarifa polisi ambao walifika usiku huo na kumchukua mtuhumiwa huyo.
“Nilikuwa nimekaa kilabuni akaja huyu kijana aliyefanya mauaji akaniuliza, Mwenyekiti ninaweza kutamka jambo ukanilinda, akasema tuongee nje, kutoka nje nikaona ana damu, akasema mimi kule nyumbani nimeua nikamwambia umeua nini hakusema akaingia ndani, nikawa na wasiwasi nikaita mgambo wakamfunga kamba na kuongozana mpaka nyumbani alikofanya mauaji ambayo ni ya babu yake” amesema Mbilinyi.
Kwa mujibu wa mwanafamilia wa marehemu Fulamu Mbilinyi, pamoja na Balozi wa mtaa huo hakukuwa na mgogoro wa aina yoyote baina ya mtuhumiwa na marehemu ambaye ni babu yake.
Kwa upande wake Daktari Nolasisi Haule kutoka hospitali ya wilaya ya Makete ambaye ndiye aliyeufanyia uchunguzi wa mwili wa marehemu amezungumzia sababu zilizopelekea kifo cha mzee huyo.
“Nimeangalia maiti,miguu iko vizuri na tumbo liko vizuri kasoro ubongo umetolewa kwenye ubongo umetapakaa nje ya mwili,yaani amevuja damu nyingi na mjukuu wake hayupo sawa ni mvuta bangi,anavuta sigara na anakunywa sana pombe”amesema Daktari Nolasisi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Hamis Issa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akieleza kuwa hatua za kisheria zitachuliwa dhidi ya mtuhumiwa sambamba na kuwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.
“Kweli tukio hili limetokea na inaonyesha huyu mjukuu hana baba wala mama na ana tabia ya kupoteza kumbu kumbu,alimvizia babu yake akampiga mti wa kichwa na kichwa kikapasuka,na imeingia imani ya kishirikina huyo kijana yuko mbaloni na hatua za kisheria zinachuku dhidi ya tukio hilo”amesema Kamanda Issa.