Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamanda Lazaro Mambosasa amekipongeza kikosi maalum kilichofanyakazi ya kulinda amani katika maeneo ya Kibiti, Rufiji, Mkuranga, na Mafia Mkoani Pwani.

Ametoa pongezi hizo mara baada ya kufanya ziara maalum kwenye kambi ya kikosi hicho kilichopo Wilayani Rufiji ikiwa ni sehemu ya ujirani mwema na kusema kuwa kazi inayofanywa na kikosi hicho matunda yake yanaonekana hadi nje ya mipaka ya Mkoa wa Pwani.

“Chini ya usimamizi wa Mkuu wa Oparesheni, Naibu Kamishna wa Polisi, Liberatus Sabas Kibiti, Rufiji hali imekuwa shwari kwani awali hali ilikuwa mbaya. hakuna asiyejua kuwa ilifika mahali watu wakawa wamekata tamaa na hata kukimbia maeneo yao na wengine wakisema Tanzania haijawahi kupitia maisha ambayo watu walikuwa wanapitia. tunawapongeza sana kwa kazi nzuri,” amesema Mambosasa.

Katika ziara hiyo Kamanda, Mambosasa ameongozana na makamanda wa mikoa ya kipolisi ya Ilala, Temeke, na Kinondoni, ambao wamesisitiza ushirikiano baina ya vikosi vya ulinzi bila kujali mipaka.

 

Video: Msimamo wa bodi ya mikopo kwa wadaiwa sugu
Sudan yatakiwa kuheshimu mkataba wa Amani