Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete ameupongeza uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kwa kuandaa mashindano ya ‘Kili Challenge’ yaliyowakutanisha wadau mbalimbali kupanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuhamasisha vita dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi.

Dkt. Jakaya Kikwete akihutubia katika ufunguzi wa 'Kili Challenge'

Dkt. Jakaya Kikwete akihutubia katika ufunguzi wa ‘Kili Challenge’

Akizungumza hivi karibuni Machame mkoani Kilimanjaro katika ufunguzi wa tukio hilo lililozikutanisha taasisi za serikali, Mashirika binafsi pamoja na wawakilishi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Kikwete aliwataka wadau kuunga mkono juhudi za kupiga vita maambukizi ya Ukimwi ili kufikia lengo la kutokuwa na maambukizi mapya, kuondoa unyanyapaa na hatimaye kutokuwepo Ukimwi.

“Ninawashukuru kwa dhati GGM na washirika wao. Huu ni ushirikiano chanya wa utekelezaji wa jukumu. Ninatoa wito kwa makamupuni mengine au hata mtu mmojammoja kuchangia katika mpango huu. Tuungane pamoja katika vita dhidi ya Virusi vya Ukimwi ili tulifanye taifa letu kuwa la kwanza duniani kuwa na kiwango cha ‘3 Zero’(Kutokuwa na maambukizi, kutokuwa na unyanyapaa na kutokuwa na vifo vitokanavyo na Ukimwi),” alisema Dk. Kikwete.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Terry Mulpeter alimshukuru Dkt. Kikwete kwa kuhudhuria katika tukio hilo. Alisema kuwa hatua hiyo imeonesha namna ambavyo amejitoa kwa dhati kuunga mkono juhudi zinazofanywa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika vita dhidi ya VVU/Ukimwi.

“Mwaka huu watu watakaoupanda Mlima Kilimanjaro katika Kili Challenge wanatoka mataifa mbalimbali. Miongoni mwao wanatoka hapa Tanzania, Mali, Afrika Kusini, Marekani, Uingereza na Australia. Kwa pamoja tutafanya tukio hili la kihistoria kwa nia njema na kwa lengo la kutimiza ndoto,” alisema Mulpeter.

Alisema kuwa wameweza kufanikisha tukio hilo kutokana na ushirikiano kati ya TACAIDS na washirika wao wengine ambao wamejikita katika kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa.

Katika mashindano hayo, kundi la watu 57 liliupanda Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi Afrika ikiwa ni pamoja na waendesha baiskeli 30.

Paul Pogba Kuvaa Jezi Namba 6 Atakapotua Man Utd
Chadema waishitaki Serikali Mahakama ya Afrika Mashariki