Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amewataka watanzania kupuuzia taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijami kuhusiana na sababu za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Media, Regnald Abraham Mengi kilichotokea Mei 2 mwaka huu, Dubai, Falme za Kiarabu.

Dkt. Kikwete ambaye leo amefika nyumbani kwa Marehemu, Kinondoni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa pole kwa familia amesema kuwa ukweli wa sababu za kifo cha Mengi wanaoufahamu ni binti yake na mdogo wake Benjamin.

Hivyo amewaomba watanzania kutulia hadi wawili hao wataporejea nchini na kueleza chanzo cha kifo chake kwani walikuwepo Dubai pindi mzee Mengi alipopatwa na umauti.

”Sisi wengine tuendelee kuwa watulivu, tuache uongo tuache kuingiza yasiyokuwepo tukaichanganya jamii,” amesema Dkt. Kikwete akiongea na waandishi wa habari baada ya kutoa pole kwa familia.

“Kama kweli tunampenda Mengi haya mengine ya uongo uongo, hadithi za kutunga hizi tuachane nazo, tusubiri ukweli, ukweli tutaupata. Alifariki Dubai mdogo wake Benjamin alikuwepo pamoja na binti yake, hao ndio wana ukweli kwahiyo hayo mengine mnayosoma-soma hayo nadhani kwa sasa yaacheni tusibiri wakirudi hao naamini watatuambia ni nini hasa kilitokea na ilikuaje mpaka kile kifo kilitokea,” Dkt. Kikwete aliongeza.

Aidha, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Sirro amesema anafuatilia yanayoendelea kwenye mitandao kuhusu kifo cha Dkt. Mengi na kwamba wameanza kufanya uchunguzi kwa kufungua ‘dokezo’ ili kubaini ukweli. Kama alivyosema Dkt. Kikwete, IGP pia aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kumpumzisha marehemu na baada ya hapo jeshi hilo litaendelea na uchunguzi wake.

 

Zidane amaliza utata kuhusu tetesi za Pogba kuelekea Real Madrid
Shamim, mumewe wakamatwa na dawa za kulevya, ‘wana mtandao wa kimataifa’