Ni dhahiri kuwa mazishi ya mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo yanayofanyika leo yatamkutanisha kwa mara ya kwanza, Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa tangu waziri huyo mkuu wa zamani ajiondoe CCM na kujiunga na Chadema.

‘Marafiki’ wa muda mrefu, wameweka msamiati tata katika jamii inayotamani kufahamu nini kitakachotokea endapo wawili hao watakutana tena baada ya kugeuka kuwa mahasimu wa kisiasa.

Siku chache baada ya Lowassa kuhamia Chadema akipinga maamuzi ya Kamati Kuu ya CCM chini ya uwenyekiti wa rais Kikwete kulikata jina lake katika mchakato wa kura za maoni kumpata mgombea urais, wawili hao tayari wamesharushiana makombora wakiwa jukwaani.

Hivi karibuni, Kikwete alisikika akisema kuwa mtoto wako anapoamua kujiunga na adui yako mpige yeye na adui zako ili umuoneshe kuwa bado wewe ni baba.

Siku kadhaa baadae, kwa mara ya kwanza Lowassa alirusha kombora la moja kwa moja kwa rais Kikwete akidai kuwa ameharibu uchumi wa nchi kwa kuwa serikali yake imesababisha mfumuko wa bei.

Leo, wawili hao wanatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza wakiwa katika pande mbili hasimu za kisiasa (Chadema na CCM). Kwa mujibu wa ratiba zilizotolewa na mamlaka husika, wanaatajiwa kukutana Moshi, katika mazishi ya mmoja kati ya waasisi wa Chama Cha Mapinduzi, Mzee Peter Kisumo.

Taarifa kutoka Moshi zimeeleza kuwa msafara wa Lowassa umezuiwa kuingia katika viunga vya eneo hilo. Moja kati ya mambo ambayo jicho la wengi linataka kushuhudia kwa ukaribu, ni nini kitatokea baada ya wawili hao kukutana licha ya ukweli kuwa msibani huwa ni mahali ambapo watu huzika tofauti zao kwa muda.

Inawezekana kabisa kuwa wataalamu wa ufuatiliaji wakafuatilia kwa karibu sana hata namna watakavyosalimiana ikiwa ni pamoja na ishara mbalimbali za mikono yao na nyuso zao. Kama hili litatokea, picha itakayopatikana itakuwa picha maarufu zaidi ya mwezi huu.

Walikuwa wanaitwa Boys II Men hadi hapa walipofikia kutofautiana kwa itikadi za kisiasa. Lakini cha msingi zaidi tukumbuke hawa ni marafiki zaidi ya marafiki wa kukutana tu kwa kuwa ‘Hawakukutana Barabarani’.

Nb: Picha kutoka Maktaba

Van Gaal Abadili Upepo Wa Usajili
Tomas Rosicky Anastahili Kisu