Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Ninje leo Jumanne Desemba 5, 2017 ameanza mazoezi maalumu ya kurekebisha upungufu wote uliojitokeza kwenye kikosi chake katika mchezo uliopita.
Kilimanjaro Stars, ilicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Libya Jumapili Desemba 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kenyatta na matokeo yakawa sare tasa katika mfululizo wa mechi za michuano ya Cecafa.
Katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Machakos Academy leo asubuhi, Kocha Ninje ameanza kufanyia kazi namna ya kukaba wakati mpira unapokuwa kwa adui au timu inapopoteza mpira.
Baada ya mazoezi hayo Kocha Ninje ameoneshwa kufurahishwa na namna wachezaji walivyoelewa na kufanya kile alichowaelekeza kukifanya ambapo amesema inaonesha dalili nzuri ya kumaliza tatizo hilo lililoonekana kwenye mchezo wa kwanza na Libya.
Katika mazoezi hayo pia walifanya mazoezi ya namna ya kufanya mashambulizi na kupandisha timu.
Kesho wataendelea tena na mazoezi kujiandaa na mchezo unaofuata utakaochezwa Alhamis kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos dhidi ya timu ya Taifa ya Zanzibar.
Kilimanjaro Stars ipo kundi A pamoja na timu za Rwanda, Zanzibar, Libya na wenyeji Kenya ambapo kabla ya michezo ya leo katika kundi hilo – Harambee Stars inaongoza kwa kupata pointi 3 katika mchezo wa mwanzo, wakifuatiwa na Libya na Kilimanjaro Stars wenye pointi 1 kila mmoja wakati Zanzibar na Rwanda wakiwa hawana pointi.