Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, ameweka bayana sababu ya kuweka kambi jijini Tanga kuwa ni kutaka kujenga ‘fiziki’ na kuwaongezea kasi wachezaji wake.

Katika maandalizi hayo, Hall amesema amepanga kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mgambo na African Sports lakini akaweka sababu za kuzichagua mechi hizo badala ya Coastal kwa kusema anataka kuzisoma mapema kabla ya kukutana nazo kwenye mechi zijazo.

“Ukiangalia hatujakutana na timu hizi, tuna mchezo na Mgambo hapahapa Mkwakwani kama ilivyo kwa African Sports pia hatujacheza nao, kwa hiyo niliona kuna kila sababu ya kuziona kipindi hiki kabla ya kukutana kwenye mechi zenyewe.

“Hakukuwa na sababu ya kucheza na Coastal, maana tumeshakutana na malengo yangu kwa sasa ni kwa wapinzani wangu wajao,” alisema Muingereza huyo.

 

Azam FC jana ilicheza mechi ya kirafiki na kutoka sare ya mabao 1-1 dhidi ya Mgambo Shooting ikiwa ni mechi yake ya kwanza baada ya kuweka kambi hiyo ya Tanga.

 

Wiki ijayo, Azam itakipiga na Simba katika Ligi Kuu Bara, kisha kuwafuata Majimaji mkoani Ruvuma, kabla ya kukipiga na Mgambo, Januari 20, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Njia Tano Za Kuepuka Msongo Wa Mawazo Kazini na Kutoichukia Kazi
Azam FC Waiumiza Kichwa Kambi Ya Simba SC