Uzito unatajwa kuwa sababu kuu iliyochangia Bondia Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ kupoteza pambano la marudiano dhidi ya Erick Katompa kutoka Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo DRC.
Jumamosi (Novemba 25), Dullah Mbabe alipoteza pambano hilo la Kimataifa lililokuwa la raundi 10 la uzito wa juu na lisilo la ubingwa, kwa pointi, lililofanyika jijini Arusha.
Hii ni mara ya pili kwa Dullah Mbabe kupigwa kwa pointi na Katompa ambapo katika pambano la kwanza lililofanyika mwaka 2021 jijini Dar es salaam, alikubali kichapo.
Bondia Selemani Kidunda amesema, Dullah Mbabe alikuwa mzito kutembea na kushindwa kurusha ngumi nzito kwa mpinzani wake.
“Kama Dullah Mbabe angerusha ngumi zenye malengo angeshinda na kulipa kisasi, alirusha makonde yaliyoishia hewani na kumpa Katompa nafasi ya kutawala pambano kwa asilimia kubwa na kushinda,” amesema.
Feriche Mashauri amesema kama Dullah Mbabe angekuwa na utulivu na kupangilia vizuri makonde aliyorusha angeshinda pambano.
Amesema Katompa alitumia udhaifu wa Dullah Mbabe na kurusha ngumi zilizompa pointi na kuibuka na ushindi kwa mara nyingine.
Kocha wa ngumi Mkoa wa Pwani, Gaudence Uyaga, amesema Dullah Mbabe anapaswa kupunguza uzito utakaomsaidia kuwa mwepesi ulingoni.
“Pamoja na kuwa bondia mzuri, Dullah Mbabe anapaswa kucheza haraka na kuacha kusubiri nafasi ya kurusha makonde wakati tayari mpinzani amemkaribia,” ameongeza Uyaga.