Mfululizo wa makosa ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na unywaji pombe kupitiliza, vimetajwa kama sababu ya uongozi wa klabu ya Simba SC kufikia maamuzi ya kumsimamisha kwa kuingo Jonas Mkude.
Juzi Jumatatu (Desemba 28), uongozi wa klabu hiyo ulitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii, iliyohusu kumsimamisha kiungo huyo, ambayo iliacha maswali mengi kwa wadau wa soka, ambao walihitaji kufahamu nini chanzo cha kiungo huyo kuwekwa pembeni, huku akitarajiwa kupelekwa mbele ya kamati ya nidhamu kujibu shutuma zinazomkabili.
Habari za awali zinaeleza kuwa nyota huyo alikunywa pombe kupita kiasi kabla ya timu yake kuvaana na FC Platinum ya Zimbabwe wakati Simba SC ikipoteza kwa kufungwa bao moja kwa sifuri.
“Mkude amekuwa na tabia za kunywa kupita kiasi hata kabla ya mechi ngumu na muhimu, licha ya kuonywa amekuwa akirudia kufanya makosa hayo hata nchini Nigeria alifanya hivyo hata Zimbabwe.”
“Pia amekuwa ni mwenye kununa kila mara kwa wachezaji wenzake na hata viongozi hivyo kwa sasa madai yake yanafanyiwa uchunguzi na yeye ataitwa kujibu,” imeeleza taarifa hiyo.
Ndani ya Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck kikosi hicho kikiwa kimecheza jumla ya michezo 14, Mkude amecheza michezo 10 akikosekana kwenye michezo minne.
Katika michezo hiyo 10 aliyocheza mmoja alianzia benchi huku tisa akianza kikosi cha kwanza ndani ya timu hiyo inayopambana kutetea taji la ligi.