Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amewaomba Viongozi wa Dini kufanyia kazi changamoto ya uanzishwaji nyumba za ibada kwenye makazi ya watu.

RC Makalla ametoa ombi hilo wakati wa Kikao cha pamoja na Viongozi wa Dini kilichofanyika ukumbi wa Anatoglo na kuwaeleza kuwa amepokea meseji na simu nyingi zikimuomba afanyie kazi changamoto hiyo.

“Viongozi wa Dini ni watu muhimu na nisingependa kulitolea kauli Wala agizo la kiserikali Jambo hili, Mimi nimewanong’oneza kile nilichoambiwa na wananchi ili tusaidiane kuweka Mambo vizuri,najua nyie mna Kamati zenu mtajadiliana na kujua namna Bora ya kulimaliza vizuri,” amesema RC Makalla.

Aidha Katika kikao hicho RC Makalla amepokea maoni kutoka kwa Viongozi wa Dini juu ya utaratibu wa machinga kufanya biashara Kwenye maeneo yasiyo rasmi hususani barabarani na kuleta usumbufu ambapo wamemuomba kulitazama jambo hilo.

Hata hivyo RC Makalla amewaeleza Viongozi hao kuwa amepanga kuanza kampeni kabambe ya usafi wa mazingira kwa lengo la kupendezesha jiji hilo huku akitoa angalizo kwa kampuni za usafi zilizopata tenda ya usafi kirafiki au kujuana wakati hawana vitendea kazi.

Kwa upande wao Viongozi wa Dini wamemshukuru Makalla kwa kuona umuhimu wa kukutana nao na wamemuahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha katika utendaji kazi wake.

Kuhusu suala la nyumba za ibada kwenye makazi ya watu wameahidi watalifanyia kazi kuanzia leo kwakuwa jambo hilo limekuwa kilio cha muda mrefu.

Macron akiri Ufaransa kuhusika na mauaji ya kimbari Rwanda
Mawaziri biashara, viwanda kukutana Arusha