Jeshi la Polisi Mkoani Arusha, limewakamata watuhumiwa 188 kwa makosa mbalimbali ikiwemo ya wizi na usafirishaji wa dawa za kulevya ambapo kati yao, wawili wamekamatwa na bunda 542 za madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni mirungi yenye uzito wa kilo 298.
Taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salvas Makweli leo Novemba 14, 2023 amesema Jeshi hilo lilifanya operesheni maalumu kuanzia Oktoba 13, 2023 hadi Novemba 13, 2023 kwa lengo la kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na matukio ya uhalifu na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.
Amesema, Novemba 12, 2023 katika maeneo ya Philips Jijini Arusha walifanikiwa kumkamata Gilbert Joseph (33), mkazi wa Sinoni Jijini Arusha na Peter Waweru (33), mkazi wa Nchi Jirani wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya yadhaniwayo kuwa ni Mirungi Bunda 542 yenye uzito wa kilogramu 298kg kwa kutumia gari aina ya Isuzu (namba zimehifadhiwa).
Aidha, ameongeza kuwa “Watuhumiwa wote wawili wanaendelea kuhojiwa, pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria na Jeshi la Polisi Mkoani humo linawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Katika hatua nyingine Jeshi hilo limetoa tahadhari kwa wakazi wa Mkoa huo kuwa makini kipindi hiki cha mvua ambazo zinaendelea kunyesha ili kuepukana na majanga yanayoweza kujitokeza.
Aidha kutokana na mvua hizo hadi sasa kwa Mkoa huo wamepokea taarifa za vifo vya watu Watano ambapo wanne tayari miili yao imetambuliwa lakini mmoja bado haujatambuliwa hivyo wananchi waliopotelewa na ndugu yao kufika katika Hospitali ya Mount Meru kutambua mwili huo.
Wananchi pia wametakiwa kuwa makini hasa na watoto wadogo ambao wanahitaji uangalizi wa karibu, lakini pia kujiepusha kupita kwenye maji ya mito midogomidogo ama madimbwi ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wao hasa nyakati za usiku.