Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania – DCEA, Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo imekamata kilo 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine katika oparesheni iliyofanyika Mikoa ya Dar es Salaam na Iringa kati ya Desemba 5 – 23, 2023.

Lyimo ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam hii leo Desemba 27, 2023 na kuongeza kuwa watu saba pia wamekamatwa kwa kuhusika na dawa hizo na wawili kati yao wana asili ya Asia na kwamba huo ni mtandao mkubwa zaidi wa dawa za kulevya.

Amesema, “kiasi hiki cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogram 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine hii ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine ambayo ni mpya katika soko.”

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani”” aliongeza Lyimo.

Aidha, amewataka Wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio hayo yametokana na utoaji wa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya.

https://www.youtube.com/watch?v=wGwoLYgKBR0

 

Azam FC waingia sokoni kusaka nyanda
Mashabiki, Wanachama Simba SC waahidiwa furaha 2024