Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un amefanya mabadiliko makubwa kwenye safu ya ulinzi wake binafsi, akiwatumbua Mkuu wa Wakala wa Intelijensia, ‘Reconnaissance General Bureau (RGB)’, Jang Kil-song na Mkuu wa Kikosi cha Ulinzi wake Binafsi (The Supreme Guard Command), Jenerali Yun Jong-rin.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na gazeti la Korea Kusini la ‘Korea Herald’, Kim alifanya mabadiliko hayo Desemba 2019, katika hali ambayo haikutegemewa kufanywa kwa mkupuo.
Nafasi ya Jenerali Yun Jong-rin ambaye alikuwa kiongozi mkuu wa vikosi vya ulinzi binafsi vya Kim tangu mwaka 2010 imechukuliwa na Kwak Chang-sik. Pia, nafasi ya Jang Kil-song imechukuliwa na Luteni Jenerali Rim Kwang-il.
RGB imekuwa ikitekeleza majukumu yote ya kiintelijensia pamoja na kudaiwa kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya wahasimu wa nchi hiyo ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kimtandao (cyber-attacks).
Hata hivyo, bado haijafahamika kwanini viongozi hao wa ngazi za juu wa ulinzi na usalama wa kiongozi wa Korea Kaskazini na nchi kwa ujumla wamebadilishwa. Gazeti hilo limeeleza kuwa Wizara husika haikuwa tayari kueleza sababu.
Kim Jong Un alizua taharuki baada ya kutoonekana kwenye sherehe za kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya babu yake, hatua iliyozua tetesi kuwa huwenda yu mahututi au amepoteza maisha.
Kwa mara ya kwanza, baada ya tetesi hizo, Kim Jung Un alionekana hadharani akiwa anakata utepe kwenye uzinduzi wa kiwanda cha mbolea. Ilikuwa siku ya 20 tangu siku ambayo hakuonekana.