Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un ametoa tamko la kwanza kwa umma tangu zilipovuma tetesi kuwa yuko mahututi akidaiwa kufanyiwa upasuaji wa moyo, na hata kupoteza maisha.
Kim ambaye amefanikiwa kuhakikisha taarifa zinazotoka ndani ya Korea Kaskazini hazipatikani kwa urahisi mikononi mwa mahasimu wake, hususan zinazoihusu Serikali yake, amepongeza timu ya wataalam waliokamilisha mradi wa ujenzi wa kituo cha utalii katika jiji la Wonsan.
Gazeti la Serikali limeeleza kuwa kiongozi huyo ametoa shukurani zake kwa timu hiyo jana, Aprili 27, 2020, huku treni zake zikiwa zimeonekana katika eneo la jiji hilo kwa kipindi cha takribani siku kumi.
Serikali ya Kim Jong-un haikutilia maanani au kujibu tetesi zilizokuwa zikisambazwa kwa kasi na vyombo vya habari vya Magharibi. Mshauri wa Rais wa Korea Kusini ndiye aliyetoa tamko la kwanza kuwa kiongozi huyo wa nchi jirani ni mzima wa afya njema.
Rais Donald Trump alipoulizwa kuhusu tetesi hizo akizungumza na waandishi wa habari, alisema binafsi haziamini na kwamba anamtakia heri na afya njema kwakuwa wana uhusiano mzuri.
Taarifa nyingine zinazoenezwa hivi sasa bila kuthibitishwa zinadai kuwa Kim Jong-un alilazimika kuwekwa sehemu maalum baada ya mmoja kati ya walinzi wake kudhaniwa kuwa ana virusi vya corona.