Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un kesho atakuwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo kuvuka mpaka wa Korea Kusini, tangu kuhitimishwa kwa vita kati ya nchi hizo mwaka 1953.

Kim Jong-un kesho anatarajia kukutana na rais Moon Jae-in kwenye mpaka wa nchi hizo, upande wa Korea Kusini majira ya saa tatu asubuhi kwa saa za ukanda huo.

 

Mazungumzo ya kihistoria kati ya viongozi hao yamelenga katika kutafuta amani ya kudumu ya eneo hilo na kusitisha mchakato wa majaribio ya silaha za kinyuklia, baada ya miaka mingi ya taharuki kati ya nchi hizo.

Hata hivyo, Korea Kusini bado ina wasiwasi kuhusu kusitishwa kwa mpango wa silaha za kinyuklia za Korea Kaskazini kwani nchi hiyo imefikia hatua kubwa kiteknolojia kwa silaha hizo, na ina vinu vingi vikubwa.

“Sehemu ngumu ya mazungumzo kati ya viongozi hao ni kuhusu makubaliano ya kuachana kabisa la mpango wa silaha za kinyuklia,” msemaji wa rais wa Korea Kusini, Im Jong – seok anakaririwa.

Huu ni mkutano wa kwanza wa aina yake kati ya nchi hizo mbili baada ya mkutano mkubwa wa mwaka 2000 na 2007. Mafanikio ya mkutano huu wa viongozi hao utaandaa njia kwa Kim Jong-un kukutana na rais wa Marekani, Donald Trump.

Mzee Majuto awatoa hofu mashabiki wake
Rais wa Ufaransa adai hakuenda Marekani kumshawishi Trump