Kim Kardashian, mke wa rapa Kanye West amekuwa na wakati mgumu wiki hii baada ya kushambuliwa kwenye mtandao kwa kuweka video ya tangazo linalohamasisha vijana kula bidhaa (dawa) itakayosaidia kudhibiti hamu ya kula katika kuondokana na unene na kuwa na tumbo ‘mterezo’.
Mwanamitindo huyo ameonja joto ya jiwe ya sehemu ndogo ya mashambulizi kama yale yaliyomuandama muwewe kati ya Aprili na Mei alipotoa kauli tata kuwa Waafrika kuwa utumwani kwa zaidi ya miaka 400 lilikuwa chaguo lao.
Kim mwenye wafuasi milioni 111 kwenye mitandao yake ya kijamii, alishindwa kuvumilia mashambulizi ya wakosoaji wake na kuamua kulifuta tangazo hilo ndani ya muda mfupi. Lakini baada ya saa kadhaa alilirudisha, huenda ni kuhakikisha anatimiza makubaliano ya mkataba wake na kampuni husika.
Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 37 amekuwa msemaji wa kampuni ya Flat Tummy yenye bidhaa hizo, kwa miezi kadhaa kwa mafanikio, lakini mambo yalimgeuka alipofikia hatua ya kutangaza bidhaa hiyo.
Mmoja kati ya watu maarufu ambao walimuandama Kim K, ni muigizaji wa kike wa ‘The Good Place’, Jameela Jamil ambaye alitweet, kwa tafsiri isiyo rasmi “labda tuachane na kutumia hizo dawa za kudhibiti hamu ya kula na tuanze kula chakula cha kutosha kuhakikisha UBONGO wetu unafanya kazi vizuri na tufanye mazoezi na kazi kwa bidii na mwisho tufanikiwe.”
Aliongeza, “Pia cheza na watoto wako. Ucheze na kufurahi na marafiki. Na hatimaye uwe na kitu cha kusema kuhusu maisha yako, zaidi ya kuwa na ‘tumbo dogo’.”
Tatizo la kuwa na tumbo kubwa au unene uliopitiliza ni moja kati ya mambo yanayowasumbua watu wengi hasa vijana, katika kutafuta suluhisho, baadhi wamekuwa wakishawishiwa kutumia dawa lakini wengine wameendelea kuhakikisha wanafuata taratibu za mlo ulio bora na kufanya mazoezi.
Kim Kardashian amekuwa akionesha jinsi anavyofanya mazoezi, ingawa ni mama watoto watatu, North, Saint na Chicago, ameendelea kuwa na mwili unaovutia na tumbo dogo.