Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen amesema hajakata tamaa na safari ya kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’, licha ya kikosi chake kupata matokeo mabaya jana Jumapili (Agosti 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Taifa Stars ilikubali kupoteza kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Uganda, na kujiweka njia ya panda katika safari ya kufuzu Fainali za CHAN zitakazounguruma nchini Algeria mwaka 2023.
Kocha huyo kutoka nchini Denmark amesema ana matumaini makubwa ya kwenda Uganda na kupanga mbinu za ushindi ambazo zitakiwezesha kikosi chake kupambanai ili kutimiza lengo la kufuzu kwenye Fainali hizo.
“Bado nina imani kubwa ya kwenda Uganda na kufanya vizuri. Nimewaambia vijana wangu huu sio mwisho wetu, kwa sababu tuna mchezo mwingine ambao utaamua hatma ya wapinzani wetu ama sisi kwenda CHAN.”
“Sijakata tamaa kabisa, nina uhakika tutajiandaa vizuri na kwenda kupambana katika uwanja wa ugenini, licha ya kuwa nyuma kwa bao moja tulilofungwa hapa Dar es salaam. Soka ni mchezo wenye matokeo ya kushangaza na imekua upande wetu kwa hapa nyumbani, lakini hata sisi tunaweza kwenda kuwashangaza Uganda kwao.” amesema Kim Paulsen
Taifa Stars itakuwa mgeni wa Uganda Jumamosi (Septemba 03) mjini Kampala, Mshindi wa jumla katika mchezo huo atakata tiketi ya kucheza Fainali za CHAN.