Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania *Taifa Stars* Kim Poulsen amewapa matumaini mashabiki wa soka nchini, kwa kusema anaamini timu yake itafanya vyema katika michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la dunia.

*Taifa Stars* imeshindwa kupata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2021), kwa kupoteza mchezo dhidi ya Equatorial Guinea na kisha kushinda mchezo dhidi ya Libya, hali iliyoifanya timu hiyo kufikisha alama 7 kwenye msimamo wa kundi J.

 Timu za Tunisia na Equatorial Guinea zimefuzu kutokea kundi J, na zinakuwa sehem ya timu 24 zitakazoshiriki fainali hizo, zitakazounguruma nchini Cameroon mwaka 2022.

Kufuatia hali hiyo Kocha Poulsen amesema, anaamini kikosi chake kitafanya vyema kwenye michuano ijayo, hasa baada ya juhudi za wachezaji wake ndani ya uwanja.

Kocha huyo kutoka nchini Denmark amesema tangu alipokabidhiwa kikosi cha *Taifa Stars* amekua akifuatilia kwa ukaribu maendeleo ya wachezaji wa Tanzania, na anaona kuna muamko mkubwa wa kujituma na kufikia malengo kwa siku za usoni.

“Nimepata picha ya kila mchezaji, nani yupo katika kiwango bora na nani yuko imara, nimewaona wote najua namna ya kwenda kuitengeneza Taifa Stars mpya itakayokuwa inamiliki mpira, kufunga na kujiamini,” amesema Poulsen

Kwenye harakati za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, *Taifa Stars* imepangwa kundi J na timu za mataifa ya Benin, Madagascar na DR Congo.

Tanzania Prisons kambini Sumbawanga
Kocha Burundi: Tanzania haikutuzidi sana