Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’Kim Poulsen amesema sababu kuu iliyoplekea kikosi chake kufungwa mabao 3-0 dhidi ya DR Congo jana Alhamis (novemba 11) ni makosa binafsi ya safu ya ulinzi.
Kocha huyo kutoka Denmark amesema makosa hayo yaliifanya Taifa Stars iadhbiwe kwa kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao tangu walipoanza harakati za kusaka nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2022.
“Kabla ya yote, Poleni sana kwa kupoteza mchezo, kwa sababu wote tulikuwa na matumaini makubwa kwenye mchezo wetu dhidi ya DR Congo. Nafikiri unaweza kuona kwenye mpira, utaadhibiwa kadri ukifanya makosa ukiwa unacheza kwenye michezo mikubwa.”
“Tulifanya kosa baada ya dakika 6 na DR Congo wakaongoza na kuanza kujiamini. Tulienda mapumziko, tukajitahidi kucheza vizuri. Tulijaribu kujipanga upya ili kuwapa presha zaidi na zaidi lakini baada ya saa 1 tukafanya kosa lingine.”
“Tukasababisha kona ambayo haikuwa na sababu ya kutokea kabisa. Lakini ninachotaka kusema ni kwamba, unaadhibiwa ukicheza michezo ya kuwania kufuzu kombe la Dunia na timu ambayo inashika nafasi ya 67 kwenye viwango vya ubora wa soka duniani. Tunapaswa kupunguza makosa yetu, hiki ndicho tunapaswa kujifunza.”
“Kila mchezo unapaswa kupata funzo, na tumejifunza kuwa ukitaka kushindana kwenye mashindano makubwa hutakiwi kuruhusu makosa ya namna hii tuliyofanya. Kuwafunga DR Congo tulipaswa kuwa kwenye kiwango chetu cha juu kabisa cha ubora na hatukuwa hivyo kwa sababu ya makosa ya binafsi.”
“Tulipata nafasi lakini tulishindwa kuzitumia, kuzibadili kuzifanya mabao. DR Congo ni timu imara na yenye uzoefu. Nataka niwaambie kutoka moyoni, wachezaji walitaka sana kucheza kwa kujitolea na tumepoteza 3-0 kwa sababu ya makosa binafsi.” amesema Kocha Paulsen
Hatua ya kupoteza mchezo wa jana Alhamis (Novemba 11), inaifanya Taifa Stars kuporomoka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi J kwa kusalia na alama 7, huku DR Congo ikipanda kwenye nafsi ya pili kwa kufikisha alama 8 na Benin inaongoza kwa kufikisha alama 10.
Taifa Stars itamaliza michezo ya Makundi Jumapili kwa kucheza ugenini dhidi ya Madagascar, huku DR Congo itakua nyumbani kuikabili Benin.