“Namshukuru Mungu kwa zawadi ya mzee Mkapa, Kazi ameikamilisha”, Ni maneno aliyoyatoa kwa huzuni kubwa Rais John Magufuli huku akitoa machozi mbele ya maelfu ya waombolezaji waliokusanyika leo Julai, 28, 2020 kutoa heshima za mwisho kwa Hayati, Benjamin Mkapa Rais wa awamu ya tatu.

Wakati akitoa hotuba yake na kueleza mchango mkubwa wa mzee Mkapa kwa maendeleo ya Tanzania na Afrika amesema hana budi kueleza jinsi maisha yake yalivyoguswa na hayati pamoja na maneno ya mwisho ambayo alimwambia.

“Mzee Mkapa alinilea kama Mtoto wake, alikuwa ni shujaa wangu, alinionesha upendo.. saa nyingine machozi yanakuja tu msinishangae sana, hata Mzee Kikwete nilimuona juzi anadondosha machozi tena Kikwete ni Kanali ila alitoa chozi kwahiyo msinishangae mimi” amesema Magufuli

Na kuongeza kuwa “Kusema kweli nilikuwa nimemzoea sana Mzee Mkapa, naamini kila Mtanzania alikuwa akifurahi na kujisikia faraja sana kila alipokuwa akimuona Mkapa pamoja na Marais wenzake wastaafu, Mzee Mwinyi na Mzee Kikwete walikuwa ni kama mapacha leo hapa Mkapa hayupo nimesikitika kuona wamebaki wawili tuu, hii inaumiza sana” 

Aidha amebainisha jinsi alivyoagana naye bila kujua ndiyo mara ya mwisho na alikuwa akiambiwa maneno ya kuagwa saa chache kabla umauti haujampata.

“Mzee Mkapa niliongea nae akiwa Hospitalini kwa simu akaniambia ‘John usiwe na wasiwasi naendelea vizuri’  sikujua kuwa maneno yake yalikuwa ni ya kuniaga,namshukuru Mungu kazi ameikamilisha” Ame ongea kwa uchungu Rais Magufuli.


Taasisi, mifuko iliyoanzishwa na Mkapa kukabili umasikini
Video: Mkapa alifariki saa tatu usiku