Katibu Mkuu  wa CCM, Abdulrahman Kinana ameendelea kumng’ang’ania mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa aliyekihama chama hicho kutokana na kutoridhishwa na utaratibu uliotumika kukata jina lake katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais wa CCM.

Ingawa imekuwa ikielezwa kuwa Edward Lowassa alikuwa na mchango wake katika CCM na hata kudaiwa kuwa alisaidia katika harakati za ushindi wa serikali ya awamu ya nne katika kampeni za mwaka 2005, Kinana amesema kuwa Lowassa hakufanya kitu chochote kizuri katika chama hicho na ndio maana waliamua kulikata jina lake.

Abdulrahman Kinana akiwa na Edward Lowassa, wakiwa makada wa CCM.

Abdulrahman Kinana akiwa na Edward Lowassa, wakiwa makada wa CCM.

Akihutubia jana katika mkutano wa hadhara jijini Mwanza, Kinana alisema kuwa Lowassa alitumikia katika wizara mbalimbali serikalini lakini kutokana na kutokuwa msafi aliondolewa mara moja katika nafasi ya uwaziri mkuu aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka miwili tu.

“Hata mwalimu Nyerere alisema Lowassa hastahili kuwa kiongozi kwa sababu ya historia yake mbaya iliyojaa ufisadi. Mimi mwenyewe nilikuwepo na nilisikia kuhusu tuhuma za rushwa za Lowassa,” alisema Kinana.

Alisisitiza kuwa CCM walimchagua mgombea urais kupitia vigezo 16 na kwamba Lowassa hakukidhi vigezo hivyo.

Hivyo, aliwataka wananchi kumpigia kura Magufuli kwa kuwa ndiye kiongozi anayefaa kuwa rais wa Tanzania.

CCM Yawataka Wananchi Kutokubali Kubaki Vituoni Kulinda Kura
Chelsea, Arsenal Zaadhibiwa Na FA