Kiungo wa kikosi cha vijana cha mabingwa wa England (Chelsea) Nathaniel Chalobah, amesajiliwa na klabu ya Watford kwa mkataba wa miaka mitano, huku ada yake ya uhamisho ikifanywa kuwa siri, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na klabu hizo.
Cholabah ameondoka Stamford Bridge, baada ya kusajiliwa kwa mkopo mara kadhaa, lakini ataendela kukumbukwa kutokana na mchango wake alioutoa msimu uliopita na kuwa sehemu ya wachezaji walioiwezesha Chelsea kutwaa ubingwa chini ya utawala wa meneja kutoka nchini Italia Antonio Conte.
Aliwahi kupata mafanikio akiwa na Watford kwa mkopo mwaka 2013, kwa kuwa sehemu ya wachezaji walioipandisha daraja klabu hiyo kutoka ligi daraja la kwanza hadi ligi kuu nchini England.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 22, alicheza michezo 15 akiwa na Chelsea msimu uliopita, na pia alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 21 ambacho kilifika hatua ya nusu fainali.
Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia kwa mkopo ni Nottingham Forest, Middlesbrough, Burnley, Reading na Napoli, akiwa na Watford alicheza michezo 42 msimu wa 2012/13, na kufunga mabao matano.