Wagonga nyundo wa jijini London (West Ham Utd) wamethibitisha kumsajili beki wa kati kutoka nchini Ufaransa Issa Diop na kumsainisha mkataba wa miaka mitano.
Diop ambaye ni mchezaji wa kikosi cha vijana cha Ufaransa chini ya umri wa miaka 21, amekubali kujiunga na West Ham Utd akitokea kwenye klabu ya Toulouse inayoshiriki ligi daraja la kwanza (Legue 1) nchini kwao.
Televisheni ya Sky Sports ya England imeeleza kuwa, dili la usajili wa beki huyo limeigharimu West Ham Utd kiasi cha Pauni milioni 21.9, na jana jumanne alifanyiwa vipimo vya afya.
Diop alitua jijini London juzi jumatatu, baada ya viongozi wa klabu za West Ham Utd na Toulouse kufikia makubaliano ya usajili wake, na anakuwa mchezaji wa pili kusajiliwa chini ya utawala mpya wa meneja kutoka nchini Chile Manuel Pellegrini.
Mchezaji wa kwanza aliyesajiliwa na meneja huyo wa zamani wa Man City alikua Ryan Fredericks aliyetoka Fulham.
West Ham Utd wamekamilisha dili hilo na kuzipiku klabu za AS Monaco, Olympic Marseille zote za Ufaransa, RB Leipzig ya Ujerumani na Sevilla ya Hispania ambazo kwa pamoja zilikua vitani zikiwania saini ya kinda huyo.
Diop anaondoka Toulouse, huku akiacha kumbukumbu ya kucheza michezo 31 msimu uliopita, na alikua mmoja wa wachezaji waliowezesha harakati za klabu hiyo kutokushuka daraja.