Wanajeshi wa Urusi waliokuwa wanadhibiti kinu cha zamani cha nyuklia huko Chernobyl Ukraine, wameondoka,
Wafanyakazi wa kinu hicho wamesema kwa sasa hakuna wageni wanaozunguka eneo hilo la kampuni ya nyuklia ya serikali ya Ukraine Energoatom.
Hapo awali, taarifa ilisema baadhi ya vikosi vya Urusi vilikuwa vimeondoka kuelekea mpaka wa Belarus, na kuacha kikundi kidogo nyuma.
Shirika la habari la Reuters liliwanukuu wafanyakazi katika kiwanda hicho wakisema baadhi ya wanajeshi hawakujua kuwa walikuwa katika eneo la mionzi na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) lilisema katika taarifa kwamba halikuweza kuthibitisha ripoti hizo.
Mkurugenzi wa IAEA alisema, hata hivyo, ilikuwa katika mashauriano ya karibu na mamlaka ya Ukraine juu ya kutuma ujumbe kwenda kwenye kinu cha Chernobyl katika siku chache zijazo.
Katika siku za hivi karibuni Urusi imesema itapunguza operesheni zake kaskazini mwa Ukraine karibu na mji mkuu Kyiv na kuelekeza nguvu zake katika eneo la mashariki la Donbas.
Siku ya Alhamisi Katibu Mkuu wa Nato Jens Stoltenberg alisema Moscow ilikuwa inajipanga badala ya kujiondoa ili kujipanga upya, kusambaza na kuimarisha mashambulizi yake huko Donbas.