Mshambuliaji kutoka nchini Gabon Emerick Aubameyang ataadhibiwa kwa kutozwa faini na uongozi wa klabu ya Borussia Dortmund kufuatia kwenda kinyume na mkataba wa kibiashara.
Aubameyang yupo haratini kutozwa faini ya Pauni 43,000, baada ya kuvaa kinyago kilichokua na nembo ya kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, hatua ambayo inakinzana na wasifu wa klabu yake ambao umejifunga kimkataba na kampuni ya Puma.
Aubameyang alivaa kinyago hicho wakati akishangilia baada ya kufunga bao katika mchezo wa ligi kuu ya soka nchini Ujerumani mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Schalke 04, ambao walilazimisha sare ya bao moja kwa moja.
Mtendaji mkuu wa Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke, ameliambia jarida la michezo la Bild kuwa: “Tabia hii ni kinyume na utaratibu wa kimkataba tuliokubaliana na wadhamini wetu, kwa hakika jambo hili huenda likavunja mahusiano mazuri yaliopo. Hatutolivumilia zaidi ya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Aubameyang.”
“Kila mmoja wetu alishangazwa na kitendo hicho, hatukitarajia kabisa lakini kwa mshangao mkubwa tuliona Aubameyang akikifanya hadharani.
“Tunafahamu anamkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike, lakini haumruhusu kuvuka mipaka ya klabu yetu, zaidi ya kuvaa viatu vyao pekee.”
Kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma, ina jukumu la kutoa huduma ya vifaa vya michezo katika klabu hiyo na pia ni inamiliki asilimia ya hisa za uendeshaji wa klabu ya Borussia Dortmund.
Hii si mara ya kwanza kwa Aubameyang mwenye umri wa miaka 27, kuvaa kinyago pindi anaposhangilia, aliwahi kufanya hivyo kwa kuvaa vinyago vya Spiderman na Batman siku za nyuma.