Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkarim Nurdin Amin ‘Popat’ ameshauri kumalizwa kwa hali ya usalama na Amani sakata la Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye amedhamiria kuvunja mkataba na Klabu ya Young Africans.
Kiungo huyo amekwama katika mpango huo kwa zaidi ya mara moja mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ ambapo mara ya mwisho alitakiwa kukaa chini na Uongozi wa Young Africans ili kumaliza sakata hilo.
Akizungumza na TBC FM Popat amesema sakata la Kiungo huyo limefikia hatua linaonekana kama kuna uadui kati yake na Uongozi wa Young Africans, halia mbayo sio nzuri kwa ustawi wa Soka la Tanzania.
Amesema kuna haja kwa viongozi wa Young Africans wakakubalia kumuachia Feisal, ili kumpa nafasi ya kucheza anapoona panafaa, na sio kufanya yanayoendelea kwa sasa.
“Mpira sio vita wala Uadui, sisi tumewaruhusu Sureboy na Gadiel Michael kwenda Young Africans wakiwa na mkataba na Azam FC, hatujawadai Young Africans wala Wachezaji hata shilingi moja, wamruhusu Feitoto aondoke.” Amesema Popat
Kuhusu usajili wa wachezaji, kiongozi huyo amesema Azam FC imefanikiwa kupambana vikali na klabu za Simba SC na Young Africans katika soko.
Amesema mara kadhaa Simba SC na Young Africans zimekuwa zikiwazidi kete kidogo kuwapata baadhi ya wachezaji, lakini hata wao kuna sehemu huwa wanafanikiwa kutokana na mahotaji wa mchezaji husika.
“Mawakala wanaosambaza Wachezaji ni hawahawa tu, Simba, Young Africans na Azam FC tunazidiana kete kidogo tu kwenye fedha, kuna Wachezaji tuliwahitaji sisi Azam waliwapata wao, na kuna Wachezaji waliwahitaji tukawapa sisi na kuna kiongozi wao alitupongeza”
“Kapombe, Nyoni, Manula, Bocco tulifanya kosa kuacha mikataba yao mpaka inakaribia mwishoni, wale hatukuwauzia Simba waliondoka huru. Hatuwezi kufanya makosa tena yaliyosababisha Wachezaji watano wakaondoka”
“Tulisajili Wachezaji wengi msimu huu na wengi wanafanya vizuri, hatutasajili sana Kuelekea msimu ujao, tutasajili Wachezaji wa (3) tu, Wawili tayari tumekamilisha usajili, bado kuwatambulisha tu, scouting yetu inafanya kazi nzuri sana hatusubiri ligi iishe” amesema Popat