Kiongozi wa kundi la kigaidi la Boko Haram, Abubakar Shekau ametoa video jana akitishia kufanya mashambulizi ikiwa ni siku chache tangu jeshi la Nigeria kutangaza kuwa limesambaratisha kundi hilo.
Katika kipande hicho cha video, amedai kuwa tamko la jeshi la Nigeria kwamba limefanikiwa kuiangusha ngome ya Boko Haram ya msitu wa Sambisa ulioko Borno sio kweli.
“Mtu anayeamini katika elimu ya magharibi ndiye tunayepigana naye vita, ambaye anaenda kinyume na imani, ndiye tunayepigana naye,” Shekau alisema kwenye video hiyo yenye dakika 11.
Video hiyo imetoka wakati ambapo jeshi la Nigeria limetangaza kuanza kujenga barabara ambayo inapita kwenye msitu wa Sambisa na kwamba inaanzisha kambi zake za mafunzo ya kijeshi ndani ya msitu huo.
Tangu mwaka 2014, jeshi la Nigeria limelidhoofisha kundi hilo linalotekeleza mauaji kwa watu wasio na hatia ingawa limekuwa likiendelea kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kuwaua wananchi.