Kongozi wa kiraia wa Myanmar aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi amepatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo jela cha miaka minne kwa tuhuma za kuleta nchini vifaa vya mawasiliano kinyume cha sheria, pamoja na kukiuka kanuni za kujiepusha na maambukizi ya corona.
Kwa mujibu wa Mahakama ya jiji kuu la Naypyitaw imeviambia vyombo vya habari kuwa Suu Kyi alihukumiwa kifungo cha miaka miwili kutokana na kukiuka sheria za uagizaji bidhaa nchini na kuleta vifaa vya mawasiliano vya walkie talkie, kinyume cha sheria, pamoja na kukiuka sheria za nchi za majanga ya kiasilia ambazo zinalinda dhidi ya maambukizi ya corona.
Hukumu iliyotolewa Januari 10, 2022 imekuja, mwezi mmoja baada ya Suu Kyi kupatikana na hatia nyingine ya kuchochea umma.
Iwapo Suu Kyi mwenye umri wa miaka 76 atapatikana na hatia kutokana na mashitaka yote yanayomkabili, basi huenda akapewa kifungo cha zaidi ya miaka 100 jela na utawala wa kijeshi uliomuondoa madarakani Februari mosi mwaka wa 2021.
Suu Kyi pia anakabiliwa na tuhuma za kutoa siri za serikali, utumizi mbaya wa ardhi pamoja na kupokea fedha zisizo halali.