Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un amejibu hotuba iliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump aliyetishia kuharibu nchi hiyo kupitia hotuba yake kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Katika hotuba yake, Trump alisema kuwa Marekani itaiharibu kabisa Korea Kaskazini kama italazimika kufanya hivyo, endapo nchi hiyo itaendelea na majaribio ya makombora ya nyuklia.

Kupitia tamko lake alilolitoa kupitia vyombo vya habari, Kim Jong –Un amekaririwa akisema kuwa Trump ataijutia kauli yake na itamgharimu.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Ri Yong-ho ameonya kuwa kiongozi wa nchi hiyo anaweza kutoa amri ya kufanya majaribio ya kombora zito zaidi la ‘hydrogen’ kwenye bahari ya Pacific.

Alisema kuwa hatua hiyo itakuwa majibu ya vitisho vya Marekani dhidi ya hatua zake za kufanya majaribio ya makombora.

“Hili linaweza kuwa kombora zito zaidi la Hydrogen kwenye bahari ya Pacific,” Ri anakaririwa na shirika la habari la Korea la Yonhap.

“Hata hivyo, hatujafahamu hatua gani hasa tutakayochukua kutegemea na maelekezo tutakayopewa na kiongozi Kim Jong-Un,” aliongeza.

Marekani na Korea Kaskazini wamekuwa kwenye mgogoro mzito kuhusu majaribio ya mabomu ya nyuklia kwenye Pwani ya Korea.

 

Video: Mbowe asema Lissu hatasafirishwa kwenda kokote
Huu ndio wimbo unaomkera Lukaku