Kiongozi wa upinzani nchini Guinea, Cellou Dalein Diallo, amejitangaza mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili kabla ya kutangazwa kwa matokeo rasmi.
Diallo hakutoa takwimu zozote lakini amesema kuwa hitimisho lake ni kutokana na hesabu ya chama chake wala sio tume rasmi ya uchaguzi na amewaambia wanahabari na wafuasi wake kwamba ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi.
Tume ya uchaguzi imejibu kwa kusema shughuli ya kuhesabu kura bado inaendelea na hiyo ndio pekee yenye mamlaka ya kumtangaza mshindi.
Wafuasi wa Diallo ambao walikuwa wamekusanyika kusherehekea walitawanywa na maafisa wa polisi.
Baada ya tukio hilo, Diallo kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika ujumbe kwamba watu watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na polisi.
Raia wa Guinea wamekuwa wakiandamana kwa miezi kadhaa sasa tangu Rais Alpha Condé alipotangaza kuwania muhula wa tatu.
Matokeo ya uchaguzi huo uliotanda wasiwasi yanatarajiwa kutolewa Jumatano na baada ya hapo wagombea watakuwa na siku nane za kukata rufaa ikiwa wana malalamiko yoyote.
Mgombea wa urais anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura kupata ushindi wa moja kwa moja ambapo iwapo atapata ushindi wa chini ya asilimia 50, kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi Novemba 24.