Maafisa nchini Belarus, wamemkamata mjumbe wa mwisho wa ngazi za juu wa baraza la upinzani waliokuwa wamebaki huru, ikiwa ni hatua ya kimfumo ya kuyamaliza maandamano yaliyodumu mwezi mmoja dhidi ya rais wa nchi hiyo, Alexander Lukashenko.
Wakili Maxim Znak, mwanachama wa baraza la uratibu lililoundwa na upinzani kusimamia mazungumzo na kiongozi wa nchi hiyo aliyekaa madarakani kwa miaka 26 sasa, alichukuliwa katika ofisi ya baraza hilo na watu wasiojulikana waliokuwa wamefunika nyuso zao.
Waendesha mashitaka wa Belarus wameanzisha uchunguzi wa jinai dhidi ya wanachama wa Baraza la Uratibu, wakilituhumu kwa kuhujumu usalama wa taifa kwa kudai uhamisho wa madaraka.
Wakati huohuo, kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo, Svetlana Tikhanovskaya, leo ameelezea matumaini kuwa mkondo wa demokrasia nchini mwake utakuwa mfupi zaidi kuliko ulivyokuwa kwa Poland wakati wa muungano wa Kisovieti.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Poland, Tikhanovyskaya amelinganisha maandamano nchini mwake na miaka mingi ya mapambano ya chama cha wafanyakazi cha Solidairity nchini Poland, ambacho kilisaidia kuuangusha ukomunisti mwaka wa 1989.
Tikhanovyskaya pia amekutana na Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki, ambaye naye pia aliandamana dhidi ya Ukomunisti, na akazungumza na Wabelarus wanaoishi Poland.