Mlinda Lango wa Mabingwa wa Soka nchini Nigeria Rivers United ya Nigeria, Victor Sochima amesema msimu ujao 2023/24 huenda akacheza soka katika ardhi ya Tanzania huku akitaja miongoni mwa timu zinazomvutia ni matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
Sochima ameonyesha kiwango bora katika michezo miwili ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Young Africans, jambo lililozifanya baadhi ya timu nchini kuanza mazungumzo naye kimyakimya.
Akizungumza na Dar24 Media kutoka Nigeria, Sochima amesema timu nyingi zimefurahishwa na uwezo wake hivyo zilimfuata kuzungumza naye ingawa kwa sasa akili yake amewekeza kuhakikisha msimu huu unamalizika.
“Siwezí kuweka wazi kila kitu kinachoendelea lakini itoshe kusema kweli nimefuatwa na baadhi ya timu ikiwemo Young Africans kwa sababu baada ya mechi kuisha nilifuatwa na kocha Nasreddine Nabi.” amesema.
Sochima ameongeza mbali na Young Africans timu nyingine ambayo imeonyesha nia ya kuhitaji saini yake ni Azam FC ambayo anatamani kuichezea kwani miundombinu iliyonayo inamshawishi tofauti na kwingine.
“Pale Azam FC kuna rafiki yangu anaitwa Isah (Ndala) ni mchezaji mzuri ambaye nimekuwa naye karibu, hivyo nitafurahia kama itatokea siku moja tutacheza pamoja ingawa kwa sasa dili bado halijakamilika.”
Wakati Sochima akiweka wazi mipango hiyo, inaelezwa kuwa Azam FC ipo kwenye rada za kutafuta kipa atakayesaidiana na Abdulai Iddrisu iliyemsajili Januari kutoka Bechem United ya kwao Ghana.
Usajili wa kipa mwingine ni kutokana na kutoridhishwa na kiwango cha Ali Ahamada ambaye tangu ajiunge msimu huu amekuwa akifanya makosa mengi ya kizembe.