Kipande cha ubao kinachoaminiwa kuwa sehemu ya vifaa vilivyotumiwa na Yesu kimerejeshwa mjini Bethlehem baada ya miaka zaidi ya 1,000 barani Ulaya.
Papa Francis aliagiza kurejeshwa kwa Kipande hicho cha ubao ambacho kilikuwa kanisa la Roma la Basilica ya Santa Maria Maggiore chenye ukubwa wa mkono wa binadamu tangu karne ya saba.
Awali kilisimamishwa kwa muda mfupi kwenye eneo la umma mjini Jerusalem kabla ya kuendelea na safari yake hadi mjini Bethlehem ikiwa ni mwanzo mwa sherehe za Krismasi mjini humo.
Kibao hicho kilipokelewa Mjini Bethlehem siku ya Jumapili na Bendi ya gwaride na kuchukuliwa katika kanisa la Mt. Catherine, karibu na Kanisa la Nativity ambako wataalamu wa masuala ya utamaduni wanasema Yesu alizaliwa.
Imeelezwa kuwa wasimamizi wa Custodia Terrae Sanctae, maeneo matakatifu ya dini za kikatoliki katika Ardhi Takatifu wanasema Kipande hicho kilitolewa kama msaada na wasimamizi wa eneo takatifu la St Sophronius kwa Papa Theodore 1 katika karne ya 7.
Kurejeshwa kwake kumekuja wakati wakristo Wakatoliki wakianza kipindi cha kujiandaa kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo kinachofahamika katika kanisa hilo lama Adventi- ,ambacho huwa ni majuma manne ya kuelekea sikukuu ya Krismasi.
Wakristo wanakadiriwa kuwa 1% ya Watu wa Palestina katika eneo la Ukanda wa magharibi (West Bank), Gaza na Jerusalem Mashariki , lakini Bethlehem ni eneo maarufu kwa mahujaji wa Kikristo kutoka maeneo mbalimbali ya duniani hususa ni wakati wa Krismasi.