Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amepiga marufuku fedha za miradi ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutumika kulipa posho kwa wasimamizi wa miradi hiyo.
Kipanga ameyasema hayo wakati alipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha VETA Butiama kilichopo Wilayani Butiama Mkoani Mara ambapo hakuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa huku fedha nyingine kiasi cha milioni 75 zikiwa zimetumika kulipa posho watu mbalimbali.
“Hizo pesa zaidi ya milioni 75 mlizolipana posho zirudishwe mara moja kwa kuwa lengo la pesa hizo halikuwa kulipa posho bali kufanyia ujenzi na kuanzia leo ni marufuku pesa za miradi ya ujenzi kutumika kulipana posho,” amesisitiza Kipanga.
Katika hatua nyingine, Kipanga amevunja Kamati za Ujenzi na Mapokezi na kuwasimamisha Msimamizi Mkuu wa mradi huo, Vedasto Rutahakana ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha VETA Mara pamoja na Afisa Manunuzi, Mwesiga Tebuka kutokana na kushindwa kusimamia vizuri mradi huo na kumtaka Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Pancras Bujulu kuhakikisha anaweka wasimamizi wengine mara moja ili ujenzi ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Aidha, Naibu Waziri Kipanga amewaomba Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Mkurugenzi wa Halmashauri, Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Butiama na Wilaya nyingine ambapo vinajengwa vyuo vya VETA kushirikiana na wasimamizi wa miradi hiyo ili kuhakikisha ifikapo Machi 31 mwaka huu ujenzi unakamilika.
Katika ziara hiyo, Kipanga pia alitembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) cha Wilaya ya Musoma na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa majengo mapya ambayo ni bweni moja, jiko, karakana nne na jengo la Utawala.