Afisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire amedhihirisha kuwa sehemu ya wadau wa soka walioguswa na matokeo ya mchezo wa Simba SC dhidi ya Kaizer Chiefs, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Simba SC ilipoteza kwa kufungwa mabao manne kwa sifuri ikiwa ugenini FNB Stadium (Soccer City) Afrika Kusini Jumamosi (Mei 15) katika mchezo wa mkondo wa kwanza, na mwishoni mwa juma hili itacheza nyumbani jijini Dar es salaam katika uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mchezo wa mkondo wa pili.

Masau amethibitisha kuguswa na kichapo hicho, kupitia ujumbe wake aliousambaza kwenye mitandao ya kijamii akianza na kichwa cha habari kinachosema KAIZER CHIEFS WAMETUGEUZA WANAWAKE, HATARI SANA HAWA WAMETUKOMESHA.

“Nilishindwa kabisa kunena, mwili ulilegea kama udenda wa usiku, yaani wapendwa , hawa Kaiser Chief,  wametukomesha!

Hii Mbungi, sijui kama tutatoboa, kwenye mpira wa miguu, chochote chaweza kutokea, ila, nauona ugumu fulani kutoboa mbele ya wajukuu hawa wa Madiba!

Jeuri yetu yote, ndoto zetu za kutwaa ubingwa wa Afrika,  ligi ya mabingwa, taratiiiiiibu, unatokomea!

Yaani,  nauona uanaume wa Kaiser Chief , na kwamba, hao tuliokutananao huko nyuma, wote wanawake, Kaiser Chief,  wametufanya wanawake, hatari sana hawa!

Poleni Watanzania wenzangu,  tugange yajayo!

Tuombe muujiza wa Mungu,  twaweza kuwafurusha, kwa kuwatia mkono hapa nyumbani!

Au ninyi Watanzania wenzangu,  mnasemaje?” >> Ujumbe wa Masau Bwire, msemaji wa klabu ya Ruvu shooting.

Kufuatia kufungwa mabao manne kwa sifuri ugenini, Simba SC itatakiwa kushinda mabao matano kwa sifuri, ili itinge hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Kamati ya Corona yapendekeza chanjo itumike kwa hiari
Rage: Simba SC inatoboa Afrika