Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto – UNICEF, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC limesema kuimarika kwa mapigano mashariki mwa taifa hilo, kumewatumbukiza watoto katika mlipuko mbaya zaidi wa ugonjwa wa kipindupindu tangu kupita kwa kipindi cha miaka sita.
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa hii leo katika mji wa Goma uliopo jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, inaeleza kuwa kumekuweko na wagonjwa 31,342 wa kipindupindu ambapo kati yao hao, 230 wamekufa kwa kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu, wengi wao wakiwa ni watoto.
Jimbo lililoathirika zaidi ni Kivu Kaskazini ambako zaidi ya watoto 8,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano waliambukizwa kipindupindu katika miezi 7 ya mwanzoni mwa mwaka huu, idadi ambayo ni mara sita zaidi ya mwaka mzima wa 2022.
Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na wagonjwa 5,120 mwaka mzima wa 2022 ambako wagonjwa 1,200 walikuwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, na iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa mapema, kuna hatari ya ugonjwa huo kusambaa maeneo mengine ya nchi hiyo.
“Ukubwa wa mlipuko wa kipindupindu na kiwango cha tishio lake vinapaswa kuwa kengele ya dharura,” amesema Shameza Abdulla, Mratibu wa dharura wa UNICEF Goma, ambao ndio mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Aidha, Abdulla amesema kuna hatari pia kuwa kipindupindu kitaendelea kusambaa kwenye makazi ya wakimbizi wa ndani ambayo tayari yana idadi kubwa ya watu hasa Watoto walio hatarini zaidi kuambukizwa magonjwa na hatimaye kifo.
Mwaka 2017 kipindupindu kilienea nchi zima ikiwemo mji mkuu wa DRC, Kinshasa na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100 kati ya wagonjwa 55,000 huku takribani watu 300,000 wakiwemo Watoto 183,000 hawana maji ya kutosha, chini ya theluthi moja wana huduma za vyoo, ikimaanisha watu 159 wanatumia choo kimoja.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na Wizara ya Afya ya Umma DRC, kati ya mwezi Mei na Juni mwaka huu kwenye kaya zenye wagonjwa wa kipindupindu jimboni Kivu Kaskazini umebaini kuwa kati ya asilimia 62 hadi 99 ya kaya hizo ni familia ambazo mwaka jana zilifurushwa makwao.